Professor Ali Mazrui, the Producer of the seminal documentary on Africa- THE AFRICANS back in the 70s died this morning October 13th .
He is a great figure in African political sciences and through the film we were able to bring Africa to the world to see us in all our glory and times.
A big big loss to Africa and mankind! Inna Lillah!!

Professor Martin Mhando, CEO ZIFF


KWAHERI YA MOYO WA SIMBA

(Kwaheri Profesa Ali Mazrui)

Wa heri Profesa mwenza, mkono nakupungia
Safari uliyoanza kiyama imefikia
Njia panda tuloshoza, kishindo tumesikia
Mti mkuu mkuukuu, kuanguka si ajabu

Foliti ulipocheza, kificho hakikushinda,
Mnazi ulipokweza, shingo juu twalipinda,
Kukuona twaliweza, na hapo twalikutunda,
Mti mkuu mkuukuu, kuanguka si ajabu

Twenda tukikutazama, nyuma tulikotokea
Si bata kajionea, uchafu alofumuwa,
Lulu na alimasi pia, wewe umetuwachia,
Mti mkuu mkuukuu, kuanguka si ajabu

Nalitazama jahazi, mbali likijitwekea,
Naziona jarifezi, samaki zimelemea,
Hazina tosha ustazi, jamii umetwachia,
Mti mkuu mkuukuu, kuanguka si ajabu

Umekuwa mgombea, haki pia usawia,
Shirika metujengea, Afrika twajiringia,
Mlizamu twajinywea, fikra zabubujikia,
Mti mkuu mkuukuu, kuanguka si ajabu

Kwaheri Mwalimu wangu, salimia walimuzo,
Tulobaki nasi chungu, twakumbuka simulizo,
Japo kwaheri ya uchungu, kilio si hitimizo,
Mti mkuu mkuukuu, kuanguka si ajabu