TUWEKE MIUNDOMBINU
MUHIMU NA SERA BORA KWANZA

Nisingependa kupoteza muda kuzungumzia jinsi Hollywood inavyoitawala dunia japo kwa sasa Marekani haina nguvu duniani. Hiyo yote ni alama ya nguvu ya filamu na television duniani na hasa ubepari unavyoubeba Umarekani.
“Hollywood also has a significant impact on global media, as American television shows and movies are widely distributed and consumed around the world. This has led to the spread of American culture and values, and has also influenced the development of media industries in other countries.” (Wikipedia)
 
Ukiacha hilo, ambalo si dogo, kutengeneza filamu kwa kutumia mandhari za Africa hakujasaidia maendeleo ya tasnia ya filamu kokote. Ukiuliza ni filamu ngapi zilizopigwa Kenya na ukiangalia jinsi sote tunavyosota leo, ndipo utakapoona kuwa kupiga filamu hakuendelezi tasnia ya nchi filamu zinakopigwa. Tofauti ya Nigeria na Kenya ni wazi kabisa na Nigeria hakuna filamu nyingi zinazopigwa kule. Mambo ni kujipanga.
 
Africa ya kusini ni nchi moja ambayo pia imechukuwa filamu nyingi zikapigwa kule. Na kwa wao si kwa sababu ya mandhari tu bali kwa kuwa wanayo miundombinu kabambe ya utengenezaji filamu na kwa njia hiyo  Hollywood wanapokwenda kupiga filamu kule, japo watu kadha wakubwa kwenye crew wanakuwa wananchi wa Sausi. Kwa hiyo kujenga miundombimu ni muhimu kama tunataka kufaidika na upigwaji wa filamu kwenye nchi fulani. 
 
Je sisi tunayo miundombinu hiyo? Tunapowakaribisha kuja huku je wanakuja kujenga miundombinu? Na hata kama watakuja je watatuwezesha kukua na kuwa wabobezi wanaowatumia? Zaidi ya hapo je mazingira ya kuwaruhusu na kuwawezesha kujenga miundombinu ni mazuri? Kwa sasa hakuna atakayekuja kuweka miundombinu hapa katika mazingira mabaya kama haya tuliyonayo. Sina tabia ya kufichaficha. Hali ya sera zinazohusu filamu nchini ni mbaya sana. Hata mangi hawezi kufungua biashara!. Na kama unabisha angalia Wachaga wangapi wako kwenye tasnia ya filamu Tanzania!
 
Wazo tofauti lilitumika Ireland. Wao walijenga miundombinu na miundombinu kababe hasa wakati teknolojia ya kidijiti ilivyoingia. Wao walijenga miundombinu ya Post-production ambayo waliifanya kuwa rahisi na rafiki kiasi ya kuwavutia watengeneza filamu wa Hollywood kwenda kule. Ni kweli walijiuza kirahisi lakini hiyo ililetea kuja kwa fedha nyingi zaidi na utengenezaji wa filamu nyingi zaidi na kwawezesha watengeneza filamu wa Ireland kukukimbilia fursa. Sasa Ireland, kanchi kadogo, kanasimama kidete mbele ya wabwanga wa sinema na wao wakaonekana.
 
Vivyo hivyo walifanya South Korea. Wao lakini walihangaika kiasi hadi kufikia walipo. Kwanza walijaribu kuwezesha utengenezaji wananchi wa filamu chache lakini za fedha nyingi. Moja au mbili zilifanikiwa lakini baada ya hapo zilizofuata zikafeli mpaka ikaonekana ni bora kubadili mwendo.
 
Wakaingia kutengeneza filamu za bei ndogo kwa msaada wa serikali nazo pia hazikwenda mbali. Lakini kwa kuwa ni bei nzuri wawekezaji wakaona ile mifumo mizuri na rafiki waliyotengenezewa na serikali inawavutia, na wanaweza kutengeneza fedha na kuwa na confidence ya kufikia soko, basi wakaingia huko. Wakaanza kutengeneza filamu nyingi kwa soko lao bila kulitazama soko la nje hasa kwa sababu miundombinu iliyokuwapo iliwawezesha kuwafikia watazamaji kwa wingi na kwa namna wanayotaka wadau. Sasa Korea wanatengeneza filamu hizo hizo kwa soko la ndani lakini nazo zinakwenda kwenye masoko ya majuu. Hawa mimi naona ni wa kuwasoma na kuangalia waliwezaje kujenga miundombinu yao, sera na mafunzo ili kufika walipofika. Sisi kutujengea chuo ni mwanzo mzuri lakini hakutatusaidia kama sera zetu za mtazamo-chongo, yaani wa mtu ambaye haoni sawasawa lakini anasema huko ndio kuona kwenyewe, na anajisifia kuwa kuwa chongo ni zaidi ya kuona na macho mawili!
 
Wengine waliojaribu njia nyingine ni Waustralia. Wao katika miaka ya 1980 waliweka sera ya kusaidia tasnia kwa kuondoa kodi. Na zaidi ya kuondoa kodi wao walifanya kuwa, mwekezaji mkubwa mwenye biashara nyingi mbali ya filamu, akiwekeza kwenye filamu anapunguziwa kodi kwa kiwango cha fedha aliyowekeza na Zaidi. Yaani 150% Tax Refund.
 
Yaani walisema kuwa, kama mwisho wa mwaka ulikuwa unatakiwa kulipa kodi ya milioni mia moja kwa biashara ya kuuza ving’amuzi I(kwa mfano Azam) basi mwisho wa mwaka fedha uliyowekeza kwenye filamu unarudishiwa yote na unapata asilimia 50% Zaidi. (yaani milioni hamsini zaidi toka TRA ya Australia!)
 
Yaani watu walichangamkia hilo mpaka ikatoka kuwa Australia ilikuwa inatengeneza filamu hadi 10 kwa mwaka ikaenda kuwa mwaka 1988 walitengeneza filamu zaidi ya 50! Kilichotokea ni kuwa tasnia ilikua kwa haraka sana na serikali ikagundua kuwa watu walikuwa wanatengeneza filamu lakini haziishi na mwisho wa mwaka wanarudishiwa fedha. Mwisho wakaondoa ruzuku hiyo na kuifanya 110%. Lakini waliendeleza mpango wa kuwapa incentive wawekezaji. Hiyo ikaletea wawekezaji kujenga miundombinu kababe kiasi ya kuwavutia watengeneza filamu wa Hollywood. Wakaja wa Hollywood kutumia miundombinu na kwa njia hiyo kukuza tasnia ya Australia, lakini si kwa kutengeneza filamu kwa ajili ya soko la Marekani.
Kwa hiyo kuwaalika wawekezaji wa Hollywood hakutoshi kuinua tasnia bila kubadilisha sera na mifumo yetu ya mtazamo-chongo. Tusisikie maneno ya watu ambao wanaisikia tasnia na kwa kuwa wamepewa nafasi za kufanya maamuzi ambayo hayawagusi wao moja kwa moja wanaweza kuamua na kushikilia maamuzi yao. Hi ni kwa sababu kwake hata yakiharibika yeye hayamgusi. Hao ndio wenye chongo lakini sisi wenye macho ndio tumewafanya wafalme. Ingawa msemo wa wahenga ni kuwa kwa “vipofu mwenye chongo ndio mfalme”. Nawasilisha.