“NAKUPENDA NDIO MAANA NAKUPIGA MKE WANGU” na BWINIBWI LA SERA WIZARANI.

Baada ya kusikiliza hotuba ya Muheshimiwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo na majibu ya Kamati ya Bunge kuhusu hotuba hiyo siku hiyo hiyo, nilielewa msingi wa msemo huo hapo ju, “Nakupenda ndio maana nakupiga mke wangu”

Maana kwa jinsi sanaa na michezo zilivyomwagiwa sifa na waziri mwenyewe, (akijifagilia na kumfagilia naibu wake pamoja na Mama) tulitarajia mengi mazuri. Tulifurahi sana kwa kutukumbusha kuwa taifa letu liko hai kwa sababu ya utamaduni wetu unaodhihirisha thamani ya utu wetu, maana utamaduni una manufaa muhimu ya kijamii na kiuchumi.

Utamaduni huboresha elimu, afya, uchumi, amani, ushirikiano, utalii, mawasiliano na ubunifu, na kwa njia hiyo kuunganisha kazi za wizara zote 9 nilizotaja hapo. Kwa elimu na afya iliyoboreshwa, uvumilivu ulioongezeka, na kwa fursa za kujumuika na wengine, utamaduni huboresha maisha na ustawi kwa watu binafsi na kwa jamii nzima.

Sasa, kwa Waziri kutozungumzia (hapana) kutotaja neno Sera nilishangaa sana. Maana sera ndio msingi wa yote yanayofanywa na wizara na serikali. Sera hutoa miongozo, zikasimamia uwajibikaji, ufanisi na uwazi kuhusu mipango ya serikali na ya kijamii. Sasa bila kuzungumzia sera mimi naona wizara inakosa mwelekeo.

Tumekuwa tunazungumzia sera ya utamaduni kwa muda sasa, hivyo tulitarajia japo tupate mwangaza tunaelekea wapi kisera katika miezi 12 ijayo. Tulichopata ni bwinibwi. Neno la Kibondei likimaanisha kimya kizito.

Tulitaraji kusikia jinsi wizara ya Tamisemi itakavyoshirikiana na wizara yetu kutambulisha na kuhakikisha kuwa yote yanayofanywa katika wizara zote yanayohusu utamaduni wa taifa letu yanasimamiwa na wizara yetu kwa njia moja au nyingine. Ndio umuhimu wa sera.

Tulitarajia kuwa sanaa itapewa umuhimu unaostahili hasa tukilinganisha nafasi inayopewa michezo katika wizara bila kutambua kuwa sanaa inafanya yote yanayofanywa na michezo kwa ubora wa mara nyingi zaidi. Tungetambua hilo tungeona kwa nini tunapowekeza bilioni 10 kwenye uwanja mmoja na taifa zima kutokuwa na kumbi au vituo maalum vya kukuzia vipaji basi taifa linakwenda mrama. Yote haya yanatokana na kutokuwa na sera tengamana, ndani ya wizara na mipango mingine ya serikali.

Wacha nikae kimya, nisiseme!